AHLU BADR

Bismillaah.

 Kila sifa njema ni za Mwenye ezi Mungu, na swala na salamu zimfikie bwana Mtume s,a,w... waba'd:

 Siku ya 17 katika mwezi mtukufu wa ramadhani ni siku ambayo kumetokea ndani yake tukio la kiulimwengu lisokaririka. Siku kama hii Mwenye ezi Mungu s.w ameiita siku ya mfarikiano, kufarikiana haki na batil, na tawhiid na shirk.
 Siku hii imeandika tarehe, na wala si kila siku hua inasajili takhe, ispokua siku hii tukio lake linastahiki kuandikwa kwa wino wa dhahabu.
 Sio kusudio langu kuandika yaliyotokea katika siku hii, wala sababu zake, wala yaliyojiri katika tukio la Badr, kwa kua wengi wetu wanayajua hayo(kama si sote) na mara nyingi tunawasikia mashekhe wakiyataja na kuyaelezea.

 Nitagusia nukta tatu tu zinazo fungamana na siku hii.
1: Ubora wa siku hii.
2: Ubora na fadhla za walioshuhudia siku hii.
3: Hukmu ya kuhuisha utajo wa siku hii katika sheria.
 Sunna ya Mwenye ezi Mungu s.w katika maumbile yake ni kupatikana kutafautiana daraja kati ya viumbe. Na sampuli za viumbe ni tatu: 1, vyenye uhai. 2, mimea. 3, jamadi.

 Mafungu haya yanatafautiana katika daraja, bali hata kila kikundi pia, kwa mfano: vyenye uhai ni ulimwengu wa binadamu, na ulimwengu wa kondoo, na ulimwengu wa mbwa na kadhalika. Utapata ulimwengu wa wanadamu ni bora kuliko wa wengine, na ndani ya ulimwengu huo pia kuna kutafautiana, kwani daraja ya msomi si kama asiyesoma, na ya nabii si sawa na ya mtu wa kawaida, na mitume daraja yao ni zaidi ya manabii, na ulul-azm ni juu ya wengine, na sayyidul-khalq s.a.w ndiye mbora wa wote.

 Ukija katika vitu vyengine pia ni mfumo huo huo, kwani kondoo wa nabii Ismail a.s ni mbora kuliko wengine, na mbwa wa As-haabul kahf ana daraja kuliko mbwa wengine, na mtende una fadhla kuliko mimea mengine (Mtume s.a.w ameufananisha na mu'min).

Na siku kama hii nayo ni katika siku zenye fadhla na utukufu katika tarekhe ya kiislamu, kwa sababu zifuatazo: 

1: Kuwepo kwake katika mwezi mtukufu wa ramadhan.
2: Kupatikana tukio la ghazwat badr ndani yake.
3: Mwenye ezi Mungu s.w ameisifu na kuiita siku ya mfarikiano.
4: Malaika waliteremka na kushirikiana na waumini katika tukio hili la badr.
5: Ndio siku iliyopatikana ushindi wa kwanza kwa waislamu.
 
Nukta yapili ni fadhla za ahlu badr.

 Tukio hili lilishuhudiwa na maswahaba waliokua idadi yao inafika 310 na bidh3, ( bidh3 ni kati ya 3 na 9), maswahaba hawa walipata daraja kubwa mpaka kusamehewa madhambi yaliopita na yatakayokuja, hata Haatwib ibnu Abi Balta3ah alipowatumia maqureshi barua kuwajulisha kua Mtume s.a.w anapanga kuwavamia, kuna maswahaba walimuita mnafiq, hata wengine wakataka kumkata shingo, lakini Mtume s.a.w akawaambia: mwajuaje pengine Allaah s.w amewaangalia watu wa badr akawaambia: fanyeni mtakalo hakika nishawasamehe. ( swahih muslim).
 Pia Nu3aymaan ibnu Bashiir swahaba aliyejulikana kwa kuchekesha, alipolaaniwa na baadhi ya maswahaba kwa unywaji wake wa pombe, Mtume s.a.w aliwakataza kumlani, na hata alipomkosea s.Othmaan wakati wa khilafa yake, s.Othman alimwambia: lau ungelikua hukushuhudia badr ungenitambua. 
 Yote haya yaonesha daraja na fadhla za walioshuhudia vita vya badr, ndio pale wazee na mashekhe wakawa katika baadhi ya dua zao wakitawasali nao ( ndipo pale tunaposikia albadiri, yani ahlu badr). 

 Namalizia makala yangu kwa kueleza hukmu ya kuhuisha mnasaba kama huu khaswa, na minasaba mengine ya kidini 3aammah.
 Mara nyingi hua tukiambiwa kuhuisha minasaba ni bid3a, kwa kua Mtume s.a.w hakufanya. Kwanza neno la kua Mtume s.a.w hakufanya sio hoja katika sheria, na hilo tutaliwekea makala yake maalum inshaallaah.

 Ama kuhusu hukmu ya kuhuisha minasaba ya kidini katika sheria ni kua yafaa na tena ni muhimu, kwa dalili zinazofwata:
1: Nabii ibrahiim a.s aliomba utajo wake udumu, na Allaah s.w akamkubalia ombi lake, ndipo pale tunapokua katika tashahhud tunaleta Assawalaatul Ibraahimiyyah. 
2: Allaah s.w anasema : (وذكر فإن الذكر تنفع المؤمنين) kumbusha kwani hakika ukumbusho unawafaa waumini. ilivyozoeleka katika lugha baada ya fi3l inakuja masdar yake. kwa mfano: أكل يأكل أكلا , ama unapotizama aya hii utapata masdar ya fi3l hapa sio, kwasababu dhikr ni masdar ya dhakara na wala sio masdar ya dhakkara kwa shadda. Inavojulikana katika qaida ya kiswarf kua fi3l inayokua na harufu tatu kisha yakati ikawa na shadda huja masdar yake kwa uzani wa taf3iil, kwahivyo kuna hekma gani Allaah s.w asiseme وذكر فإن التذكير تنفع المؤمنبن؟ , mashekhe zetu wanatuambia hapa Allaah s.w anataka kutujulisha umuhimu wa ukumbusho wenyewe, na kua ukumbusho una uzito kuliko kukumbusha, kwasababu unaweza ukamkumbusha mtu lakini asikusikilize, ama kukiweko ukumbusho wenyewe wengi watakumbuka bila hata kukumbushwa. 

 Wallaahu a'lam.