HIJRA

DARSA NA MAZINGATIO YANAYO PATIKANA KATIKA HIJRA

 Qarne kumi na tano zilizopita kulipatikana tokeo adhimu na safari tukufu, tokeo ambalo lilibadilisha muelekeo likama ni sababu ya nusra baada ya tabu na misukosuko kwa muda wa miaka kumi na tatu.
 Kwa hakika hakuna asielijua tokeo kama hili, nalo ni tokeo la kugura Mtume s.a.w kutoka Makka kuenda Madina. Mwenyezi Mungu s.a.w aliwajaza maanswaar huko Madina mahabba ya dini ili mji huo uweze kupokea ndugu zao katika uislamu na kumpokea mtukufu wa daraja Mtume s.a.w na uwe ndio mji ambao kutaweza kuwekwa misingi ya dola ya kiislamu.
 Kisa cha Hijra ni maarufu, na ndio tukapendelea kuashiria mazingatio na darsa ambazo tunazipata katika tokea kama hili. Darsa zinazopatikana katika Hijra ni nyingi, ispokua tutachegua baadhi kutokamana na kiasi cha makala.
 Maana ya Hijra:
 Hijra katika lugha maana yake ni kugura kutoka sehemu kuenda nyengine. ama kiupande wa sheria Hijra ina maana pana zaidi ya hio, nayo ni kugura kila kibaya kuenda katika kila kizuri, kugura madhambi na maovu, kugura shawha za nafsi, kugura mikao isiyomridhisha Mwenyezi Mungu s.w. 
 Na ndio Mwenyezi Mungu s.w akampa ilhamu sayyidna Omar kuchagua mnasaba huu wa Hijra kua ndio mwanzo wa tarekhe ya kiislamu. Alikua anaweza kuchegua mazazi ya Mtume s.a.w ama siku ya badr ama siku ya kufungua Makka ama masaba wowote ule, lakini amechegua Hijra ili kila mwaka mpya ukiingia muislamu apate kugura tabia mbovu alokua nazo mwaka ulopita na maasi alokua akiyafanya. kama mtu alikua haswali basi aswali, na kama alikua aswali peke yake basi aswali kwa jamaa.
 Ndipo pale mashekhe na wanazuoni na waja wema walotangulia walikua wakiweka vikao khaswa unapofika mnasaba kama huu kukumbusha umma tokeo hili tukufu na mambo yalojiri ndani yake na matunda yalopatikana kupitia tokeo hili. Na kwakua ni siku miongoni mwa masiku ya Mwenyezi Mungu s.w, naye katika Qur'an ametuamrisha tukumbushane masiku yake.
 Darsa ama masomo yanayopatikana katika Hijra:
1: Subira huvuta kheri.
 Baada ya mateso yalompata Mtume s.a.w na maswahaba wake kwa muda wa miaka 13 mpaka kula nyasi, Mwenyezi MUngu s.w akawaandalia safari ya kugura kuenda Madina kula matunda ya subira yao katika njia ya haki, na daima wanaoshughulika na da'wa yatakikana wajue njia hio ina misukosuko, lakini anaesubiri na akawa na yakini na Mola wake basi mambo humuendea kwa uzuri mwisho. Sayyidy Ibnu Atwaaillaah asema katika hikma zake: mwenye kua na mwanzo wa tabu, hua na mwisho wenye kung'ara.
 Allaah s.w amechukua ahadi kua atainusuru dini yake na atawanusuru Mitume wake na waumini, imekuja katika surat ghafir aya ya 51: {إِنَّا لَنَنْصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ} , Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watakapo simama Mashahidi.
2: Tawakkul.
 Mu'min namna atakavopatwa na shida ataikana asiwache kumtegemea Mwenyezi Mungu s.w, Mtume s.a.w ametoka katika safari hii ya Hijra akiwa amezungukwa na hatari pande zote, lakini yote hayo hayakushutua kwa kua alikua anamtegemea Mola wake s.w. 
 Nje ya nyumba alikua amezungukwa na mashababu 40 wanataka kummaliza, na wenye kumtafuta wanafika mpaka kwenye pango na kusmama katika mlango, na Suraqa anawafata nyuma na silaha zake mpaka anamkaribia na kusikia kisomo cha Mtume s.a.w. lakini Mtume s.a.w pamoja na yote hayo alikua amejaa tawakkul na anamtegemea Mola wake s.w na akiwa na hakika kua atamnusuru. Allaah s.w anatwambia katika suratut twalaaq aya ya 3: (وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ), Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha.
3: Mahaba yanaliza.
 Katika masomo tunayoyapata katika Hijra ni somo la mahaba, mahaba ndio yalomliza sayyidna Abubakkar alipoambiwa na Mtume s.a.w kua atakua naye katika safari. Mahaba ndio yalomfanya astahmili maumivu ya kuumwa na nyoka katika pango ili asimuamshe Mtume s.a.w. Mahaba ndio yalowatoa answaar katika nyumba zao kila siku wasubiri kutokeza kwa Mtume s.a.w ili wamkaribishe katika mji wao, pamoja na joto kali lilokua siku zile.
 Kweli hakukosea aliesema: mahaba hujenga midume, mahaba hufanya yasofanywa na chengine chochote. N kwanini wasifanye hivo na nyoyo zao zilikua zimejaa mahaba. Mtume s.a.w asema: 
" لا يؤمن أحدكم حتى أكون أحب إليه من ولده ووالده والناس أجمعين ", Haikamiliki imani ya mmoja wenu mpaka anipende mimi zaidi ya mzazi wake na mtoto wake na watu wote. Na kwakua mahaba ndio yanaokamilisha imani, na imani huzidi na kupungua, basi imani huzidi kwa kuzidi mahaba na hupungua yanapopungua.
 Na kwanini tusimpende Mtume s.a.w na yeye amekusanya sababu zote za kupendwa. wanazuoni wanasema mu hupendwa kwa mambo matatu: uzuri, utukufu na akifanya wema. katika uzuri hakuna anaempata Mtume s.a.w, ama upande wa utukufu basi hamna kiumbe kitukufu zaidi ya Mtume s.a.w, na upande wa kufanya wema sema utakalo, kwani hakuna alotufanyia wema katika dunia hii zaidi ya Mtume s.a.w, ametutoa katika kiza cha ujinga na shirki akatutia katika mwangaza wa ilimu na imani. Na bado kesho qiyama atakuja kutushufaia mbele ya Mwenyezi Mungu s.w.
 Na ndio akastahiki kupendwa kwa sampuli zote za mahaba, Imam khatwabi asema: sampuli za mahaba ni tatu, mahaba ya kutukuza, mahaba ya kurehemu na mahaba ya kufanyiana wema. mahaba ya kutukuza ni mahaba ya mtoto kwa mzazi wake, na mahaba ya kurehemu ni ya mzazi kwa mtoto wake, na mahaba ya kufanyiana wema ni kati ya watu na wenzi wao, na Mtume s.a.w amekusanya sampuli zote tatu katika hio hadithi iliopo juu akasema haikamiliki imani ya mmoja wenu mpaka anipende zaidi ya mtoto wake na mzazi wake na watu wote

4: Rafiki ni mvutaji.
  Baada ya kutoka amri ya kugura kuenda Madina, sayyiduna Abubakkar kila akimwambia Mtume s.a.w yuwagura, Mtume s.a.w humwambia subiri huenda kukawa na kheri. Ikaja kheri kubwa ambayo ilimfanya sayyidna Abubakkar alie kwa kuifurahikia, nayo ni kua rafiki ya Mtume s.a.w katika hio safari.
  Kuchagua rafiki ni kitu muhimu sana katika dini, kwasababu mtu hufata tabia za rafiki yake, Mtume s.a.w asema katika hadithi iliopokewa na Imam Ahmad kutoka kwa Abu hurayra radhi za Allaah ziwe juu yake: " المرء على دين خليله ، فلينظر أحدكم من يخالل ".
  Roho ya mwana adamu ni kama upepo, upepo ukipita sehemu yenye kunukia nao hunukia, na ukipita sehemu yenye kunuka nao hunuka, na mtu pia akishikana na rafiki mzuri nae hua mzuri, na wahenga walisema: ukifatana na mvuvi utanuka samaki. na wenye hikma walikua wakisema: rafiki ni mvutaji, ima atakuvuta peponi ama atakuvuta motoni.
 Na ndio Allaah s.w katika wasia wake katika Qur'an alituhimiza kushikamana na watu wema akatuambia katika surat attawba aya ya 119: {يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ}, Enyi mulioamini mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wema.

5: Hukmu ya zefe na dufu katika sheria.
  Mtume s.a.w alipowasili mji wa Madina alipokewa na mjumuiko mkubwa wa watu, waume kwa wake, wadogo kwa wakubwa, huku wakipiga matwari. Mtume s.a.w hakuwakataza kumpokea kule kwa zefe wala hakuwakataza kupiga matwari, bali hadithi zinazozungumzia matwari ni nyingi hazina idadi, na katika hadithi mashuhuri ni ile ilioko katika swahih ya Imam Bukhari sayyiduna Abubakkar alipoingia kwa Mtume s.a.w akakuta vijakazi wakipiga matwari, akataka kuwakataza, Mtume s.a.w akamwambia waache ewe Abubakar.
  Ikiwa waliokua zama za Mtume s.a.w walimpoke na kumfurahikia kwa zefe, na sisi pia yanapofika minasaba kama hii ya mwaka mpya na pia mazazi ya Mtume s.a.w humfurahikia kwa zefe na matwari. 
  Mwisho yataka tujue kila mwaka ukituacha umri wetu unapungua na nafasi ya kufanya mema yazidi kupungua, bali kila sekunde inayopita katika maisha yako ni upungufu katika umri wako, kila mmoja katika sisi atakikana apatilize kufanya mema katika maisha yake, apate funzo namna masiku yanavokimbia, ajue kitakachomsaidi mbele ya Mwenyezi Mungu s.w kesho ni amali yake.
  Mungu atuwezeshe kukhitimisha mwaka kwa amali njema, ana aturuzuku mwisho mwema.