LEYLATUL QADRI

Laylatul Qadr kilugha, maana yake ni usiku wenye nguvu au usiku wenye kudra au usiku wa cheo kitukufu, ni usiku maalum ambao unapatikana mara moja tu katika kila mwaka ndani ya mwezi wa Ramadhani. Huu ni usiku ambao Mwenyezi Mungu anatuambia  katika kitabu chake kitukufu kuwa Qur’ani imeteremshwa katika usiku huu:-

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ

Hakika Sisi tumeiteremsha (Qur'ani) katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu.

Kama tunavyofahamu kuwa Qur’ani ni kitabu ambacho kina faida nyingi ndani yake ikiwa ni pamoja na kuwa ni muongozo kwa wenye taqwa, ni shifaa kwa wenye kuiamini, ni maelekezo ya maisha sahihi kwa wenye kukifata ni chanzo mama cha sharia za Mwenyezi Mungu kwa waislamu na wanaadamu kwa ujumla.
Bila shaka usiku huu unastahiki kuwa na hadhi kubwa. Kuhusu uteremkaji huo wa Qur’ani Ibn Abbas (radhi za Allaah ziwe juu yake) anasema:-

Allaah ameishusha Qur’ani yote ikiwa imehifadhiwa kwenye al Lahwul mahfudh kwenda kuwekwa kwenye Baytul ‘izza ambayo ipo kwenye mbingu ya dunia. Kisha ikaletwa kwa Mtume sehemu baada ya sehemu kwa mujibu wa matukio kwa muda wa miaka ishirini na tatu.

Mtume rehma na amani juu yake ameuzungumzia usiku huu katika hadithi mbali mbali. Kama hii ilivyosimuliwa na Abuu Hurayra:-

 عن أبي هريرة ، قالَ : كَانَ رسولُ اللهِ صلي الله عليه وسلم يُبَشِّرُ أصْحَابَةُ ، يقولُ : " قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضانَ شَهْرٌ مُبَارَكٌ فَرَضَ اللهُ عليكم صِيَامَهُ ، تُفَتَّحُ فيه أبوابُ الجَنَّةِ ، وَتغلَّقُ فيه أبوابُ النَّارِ ، فيه لَيْلَةٌ خَيْرٌ من ألفِ شَهْرٍ ، مَن حُرِمَ خَيْرَها فقد حُرِمَ "

Kutoka kwa Abu Hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema: Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) alkua akiwabashiria maswahaba zake akisema: “Umekujieni mwezi wa Ramadhani, mwezi wenye baraka, Allaah amekufaradhishieni ndani yake kufunga, hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na hufungwa milango ya moto, ndani yake kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu, atakaekosa kheri zake basi amenyimwa”.

Pia ubora wa usiku huu umethibitishwa katika Qura’ni pale Mwenyezi Mungu‘ anapotuambia:-

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ

Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu.

Huteremka Malaika na Jibril katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi, huteremka kwa kila jambo la kheyr na baraka.

Mbali na kuwa na ubora kuliko miezi elfu pia kwa idhini yake Mwenyezi Mungu huteremshwa malaika katika usiku huo kutokana na wingi wa kheri za usiku huo. Vile vile Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) ameuzungumzia usiku huu kuwa ni usiku wa kusamehewa dhambi, kama ilivyoelezewa katika hadithi ifuatayo:-

عَنْ  أَبِيْ هُرَيْرَةَ  رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهُ ‏عَنْ الْنَّبِيِّ  صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  قَالَ  مَنْ قَامَ لَيْلَةَ الْقَدْرِ إِيْمَانا وَاحْتِسَابا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ

Kutoka kwa Abu Hurayra kwamba amesema Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) : “mwenye kusimama katika laylatul qadri kwa imani na kutaraji malipo atasamehewa dhambi zake zote zilizotangulia.

Kusamehewa dhambi ni kitu ambacho kila binadamu anakihitaji kwa vile sote ni watenda dhambi. Hii ni neema kubwa kwa Waislamu kwa hiyo hatuna budi kujitahidi kusimama kwenye ibada katika kuutafuta usiku wenye ubora wa hali ya juu na neema nyingi.

Usiku huu unapatikana katika usiku witiri wa kumi la mwisho la mwezi huu ambapo sasa zimebaki siku chache tu kama anavyotuthibitishia Mtume (rehma na amani ziwe juu yake):-

 عَنْ عُبَادَةَ بْنِ الصَّامِتِ , أَنّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ , قَالَ : " لَيْلَةُ الْقَدْرِ فِي الْعَشْرِ الْبَوَاقِي , مَنْ قَامَهُنَّ ابْتِغَاءَ حِسْبَتِهِنَّ فَإِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ , وَهِيَ لَيْلَةُ وِتْرٍ تِسْعٌ أَوْ سَبْعٌ أَوْ خَمْسٌ أَوْ ثَلاثٌ أَوْ آخِرُ لَيْلَةٍ “ .

Kutoka kwa  Ubada bin As Swaamit (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) Hakika Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) amesema: “Laylatul Qadr inatokea katika mwezi wa ramadhani katika kumi la mwisho, mwenye kusimama kwa imani na matarajio basi hakika Allaah atamsamehe dhambi zake zote zilizotangulia, nao ni usiku mmoja katika masiku ya witiri, tisa au saba au tano au tatu au usiku wa mwisho.