ILI MUPATE KUWA WACHA MUNGU

بسم الله الرحمن الرحيم

Kila jinsi ya sifa njema astahiki Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote, swala na salamu zimfikie kipenzi chetu Mtumi Muhammad bwana wa viumbe wote.

Tukiwa mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, yafaa tujiulize kwanini kila mwaka twafanya ibada ya swaum na hatufkii wengi wetu lengo la swaum, kwa hakika ni jambo lakusikitisha mno ni mtu kufanya Jambo moja kila mwaka na akawa hafikii lengo kubwa la swaum na Ramadhani ikatoka bila ya kuwa na mabadiliko yoyote.

Kila mtu anajua kuwa Mwenyezi Mungu ametuambia wazi wazi lengo la kufunga saumu ya Ramadhani  ambalo ni uchamungu/taqwa. Na tumeshafunga Ramadhan Mara nyingi sana ! Miaka mingi ! Wengine miaka 10 , wengine 20, wengine 30 ni !

Suala ni : KWA NINI HATUFIKII LENGO HILO ?

Mwenyezi Mungu amtueleza wazi wazi kwa kusema  ( لعلكم تتقون )
ILI MPATE KUWA WACHAMUNGU !
Kwa nini hatuwi wacha Mungu baada ya RAMADHANI ??

Moja Kati ya mambo mengi tunayoyakosea ni kuwa hatuna matayarisho ! Kila jambo linahitaji matayarisho, Mwanafunzi aliyejitayarisha kwa ajili ya mtihani hawezi kuwa Sawa na Yule asiyejitayarisha ! Timu ya mpira, iliyokaa kambini kufanya matayarisho kwa ajili ya mashindano haiwezi kuwa Sawa na ile iliyokosa matayarisho , hivyo matayarisho au kujiandaa ni jambo muhimu sana katika kila kitu, na khasa katika mambo makubwa ya kumpatia mtu pepo ya Mwenyezi Mungu Kama swaum !

Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia kuingia mwezi wa Ramadhaan kwa kujiandaa kupanga mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera.  Wengi hukimbilia kwenda sokoni kununua nguo za Idi, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaan katika televisheni ambavyo sio vya dini kama 'misalsal' (maonyesho ya sinema yanayoendelea [series]), na pia kuanza kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa Ramadhaan. Pia wengine hununua karata, dumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika mchana wa Ramadhaan ili wasiihisi Swaum au kuupeleka muda haraka kama wanavyoamini wao. Haya ni makosa ! Hii ni khasara, Hii ni Moja ya sababu za kukosa kupata lengo la saumu .Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya ziada, kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na mafunzo mbalimbali ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa wepesi na kadhalika.
Huu ni mwezi wa kufanya ibada na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu zangu, tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:

Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu.

Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja Inshaallah .

Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo.

Anza mpango wako Leo  na kama unahitaji kurekebisha mpango na  nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua mpango upi au nidhamu  itakayowafikiana na hali yako. Tutapendekeza nukta Saba muhimu za kufuata in-Shaa-Allah !

MOJA: Jifunze ya mambo yanayohusu Swaum (Fiqhi ya kufunga), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako.  Jifunze Swaum kama aliyokuwa akifunga Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) ndio mfano bora kabisa wa kuufuata.

Swaum haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) amesema:

 “Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji” [Al-Bukhaariy]

MBILI: Tia nia ya kufanya mambo ya Kheri.
Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi.
Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu na jamaa.
Kama inakupasa kutoa Zaka, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii pia.
Weka azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu.

Amesema Mtume (rehma na amani ziwe juu yake): “Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga” [Ahmad, An-Nasaaiy ]

TATU: Fanya dhikri kwa wingi.
Usiache ulimi wako na moyo wako kuwa mtupu bila ya kumtaja Mola Mtukufu kila wakati kila mahali. Huku unafanya kazi zako za jikoni, fanya Adkhaar za Tasbiyh (Subhaana Allaah), Tahliyl (Laa ilaaha illa-Allaah), Tahmiyd (AlhamduliLLaah), Takbiyr (Allaahu Akbar). Kufanya hivi utajichumia thawabu maradufu, kwa kutimiza wajib wako na kuongezea kumtaja Mola wako na juu ya hivyo kuongeza baraka katika kazi zako.

NNE: Hudhuria Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha, Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa katika kuzidisha imani yako, Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku. Tumia muda wako hata wakati unafanya kazi zako za nyumba na za jikoni huku unasikiliza mawaidha. Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni halipendezi ni bora utazame na kusikiliza mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza elimu yako.
Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumkumbuka Mola wako  kwa kila aina ya ukumbusho, na mawaidha na darsa za dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa cha kutakasa Moyo na Nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Mola Wako Mtukufu.

TANO: Ikhusishe Ramadhani na Quran.
Jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur’an kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur’an na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl kwa Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) kusoma naye Qur’an yote:

Kutoka kwa Ibn Abbaas ra kwamba: Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur’an))  [Al-Bukhaariy]

Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo:

*Kusoma Qur-aan katika Ramadhaan.

*Kukutana kwa ajili hiyo.

*Kupima hifdh yako ya Qur’an kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu *nzuri ya Qur’an kwa kukusikiliza au kukufundisha.

*Kuongeza juhudi za kusoma Qur’an zaidi katika mwezi wa Ramadhaan:

Katika muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur’an kusoma na kujifunza maana ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur’an, Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura ndogo ili ukitoka katika Ramadhaan uwe una surah zaidi za kusoma katika Swalah zako.

SITA: Fanya Tawba na Istighfar.
Katika mwaka mzima ni Mara nyingi uliteleza, Omba Tawbatun-Nasuuha kwa Mola wako , wako wengi nduguzo uliowakosea waombe msamaha na kubali kuwa wewe si mkamilifu Bali ni mwenye kukosea, Kufanya hivi kutanufaisha zaidi Swaum na Swalah zako na  pia kukupa imani kuwa huna haki ya mtu.

SABA: Mwisho kabisa Omba dua kwa Mwenyezi Mungu Kama alivyokupa uhai kufikikia Ramadhan na akuwafikie kuyafanya mema, na hivyo ndivyo walivyokuwa wema waliotangulia.

Na hivyo weka maazimio ya kuendelea hata baada ya Ramadhaan kuwa katika twa'a na ibada, na kuendeleza Qiyaamul-Layl (Swalah za usiku), kusoma Qur’an japo kidogo KILA SIKU, na iwe umefungua UKURASA MPYA wa maisha yako na kumuomba Mwenyezi Mungu Akuendeleze katika hali hii.

Tumuombe Mwenyezi Mungu atuwafikie kwa kufanya kila jema katika mwezi Huu na kuacha kila lililo baya .