Rangi na sifa za heidh

 Bismillaah.


 Darsa la kwanza:


  Rangi na sifa za heidh:


 Tumependelea kuanza na heidh kwakua ni mfumo wa wanazuoni wa fiqhi katika vitabu vyao na pia ndio inayopatikana kwa wingi na kwa kila mmoja katika banati za Hawaa takriban.


 Heidh ni damu ya ada inayomtoka binti wa hawaa, na damu kama hii sio ugonjwa, ni maumbile ya Mwenyezi Mungu s.w na ni afya kutokamana na alivyoumbwa mwanamke.


 Heidh haimtoki bint wa Hawaa pekeyake, bali kuna viumbe vyengine vinavyotokwa na heidh pia, kama sungura, popo nyundo na fisi, na yasemekana pia farasi na ngamia na mbwa na bata.


 Rangi za heidh:


 Heidh ina rangi tano: 
1: Nyeusi. 
2, Nyekundu.
3, Kisasa (blond). 
4: Manjano . 
5: Hudhurungi.


 Sifa za heidh:


 Sifa zake muhimu ni kua huenda ikawa nzito, na huenda ikawa kama iloungua kwa umoto wake mkali, na hutoka kidogo kidogo wala haimwaiki, na ina harufu mbovu.


 Rangi ya manjano na hudhurungi wanazuoni wanasema sio damu, bali ni maji. 


 Pengine mtu atauliza: mbona umezitaja katika sampuli ya damu? 
 Jawabu: kwasababu wanazuoni wamesema rangi hizo zikitoka siku za ada basi moja kwa moja hua ni heidh.


 Uzindushi: kuna umuhimu mkubwa sana mwanamke wa kiislamu kujua kutafautisha kati ya rangi za damu na pia kujua mwanzo na mwisho wa ada yake kwa upande wa idadi na upande wa wakati pia. 


 Usipojua hayo basi utasumbuka kwa hukmu nyingi kama tutakavyoona huko mbele tukiashiria hukmu za wasojua kutafautisha.
 Wallaahu a'lam.